Sifa Bainifu za Fiqhi katika Kipindi cha Banu Umayyah
Wanazuoni
na wanafunzi katika dola ya Kiislamu katika kipindi hiki waligawanyika
katika makundi mawili makubwa. Kundi moja la wanazuoni liliegemea katika
upande wa kutoa maamuzi kwa kutumia Qur-aan au Sunnah, wakati kundi
jingine lilifadhilisha kutumia ukubwa wa maamuzi ya kirai na Ijtihaad.
Kundi
la kwanza lilikwepa kutoa hukumu za kisheria katika mambo ikiwa matini
ya dhahiri kutoka kwenye Hadithi au Qur-aan inayohusiana na jambo hilo haipo. Msimamo huo uliegemezwa na maana ya wazi ya aya ya Qur-aan:
وَلاَ تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ
“Wala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo” (17: 36).
Kanuni ambazo malengo yake yalitambuliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) au Mtume Wake (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yalitumiwa katika Qiyaas ilhali zile zilizoachwa bila kuelezwa hazikutumiwa. Kwa sababu ya msimamo huu, wanazuoni wa tapo hili la kifikra waliitwa Ahlul-Hadiyth (Watu wa Hadithi). Kituo kikuu cha wanazuoni wa Ahlul-Hadiyth
kilikuwa ni Madiynah na Fiqhi ya shule ya Madiynah ilikuwa kwa sehemu
kubwa, ni Fiqhi ya kimatendo na ikiegemea katika msingi wa matatizo ya
hakika.
Kundi lengine la wanazuoni walihisi kuwa kanuni zote kadhaa zilizoteremshwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zilikuwa
na mantiki, japo yawezekana mantiki hiyo imeainishwa na Allaah na Mtume
wake au la. Katika hali ambazo sababu za kanuni hizo hazikuainishwa kwa
maelezo, wanazuoni hawa walitumia juhudi zao za kiakili ili kufikia
mantiki muafaka. Baadae walitumia kanuni hizo kwa hali nyenginezo
zilizokuwa na mantiki kama hizo. Mwelekeo wao uliegemezwa na matendo ya baadhi ya Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wakubwa ambao walifikia hitimisho kwa kutoa sababu kwa baadhi ya kanuni za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Kundi hili ambalo liliunga mkono utumiaji wa akili kwa kiasi kikubwa, walikuja kujulikana baadae kama Ahlur-Ra-ay (Watu wenye kutumia Akili). Kituo cha wanazuoni wa Ahlur-Ra-ay kilikuwa ni Kuufa, Iraq.
Fiqhi ya Kuufa ilikua katika mipaka ya nadharia na dhana zaidi (isiyo
na uhakika). Matatizo yalibuniwa na mbeya tofauti za hali zilizokuwepo
kukisiwa, kisha utatuzi wa kubuni kufanyiwa kazi na kuandikwa. Katika
majadiliano yao walikuwa mara nyingi wakitumia ibara, “Ingekuwaje lau ingekuwa hivi?” na hivyo walipatiwa pia jina la utani “Ingekuwaje”. Inatakiwa ifahamike kuwa mielekeo hii ilikuwa ni upanuzi wa mielekeo iliyotokea mwanzo miongoni mwa Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum).
No comments