Header Ads

Cup of coffee on saucer

Je KUFUNGA MIKONO WAKATI WA SALA NU SUNNA AU BIDAA?

Image result for kufunga mikono katika sala ni sunna au





























Shukurani zote ni kwa Allah mtukufu na rehma na amani ziwe kwa Mtume wetu Muhammad na kila aliyeongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya malipo.Ama baada ya hayo.Tumepokea tuhuma dhidi ya ibadhi, nayo inasema kuwa Ibadhi wanapinga Sunna ya Mtume (s.a.w) kwa kutonyanyua mikono katika sala na kutoifunga, na kuwa hawana dalili katika kuachia mikono bila ya kuinyanyua na kuifunga katika sala.Jawabu:Kwa hakika suala hili ni suala la kifiqhi, nalo:
  1. Lina khilafu nyingi ndani yake kwa wenye kulithibitisha, na khilafu hiyo inaonesha udhaifu wake.
  1. Makubaliano ya wenye kulithibitisha, kuwa hayo si katika matendo ya lazima katika sala; kwani mwenye kuyawacha hayo sala yake itakuwa sahihi bila ya wasi wasi wowote, na bila shaka kujiondoa katika khilafu ni bora kuliko kukita ndani yake.
  1. Kwa hayo inabainika kuwa Ibadhi wapo katika yenye usalama zaidi, na kuwa wako nje ya yale yenye wasi wasi na mizozano ndani yake, amesema Samaahatu Sheikh Al-Khalili (h.a): ((Na ujuwe kuwa njia ya walio upande wetu (Ibadhi) katika sala ni kuchukuwa hadhari kubwa kwa kutochukuwa isipokuwa mapokezi yasiyofikiwa na wasi wasi wowote katika masuala yenye tofauti ndani yake; kwa sababu sala ndiyo nguzo ya pili katika nguzo za Uislamu, nayo ndiyo nguzo inayofuatilia baada ya Itikadi moja kwa moja, na wenye kuhakikisha katika wanavyuoni -juu ya kutofautiana kwa madhehebu zao- hawakuibali hadithi Aahadii (iliyothibiti kwa kudhania) kuwa ni hoja katika masuala ya kiitikadi; kwa kutopatisha kwake uhakika wa yakini, basi ikawa sala iliyo jirani ya itikadi kiutaratibu ina haki zaidi ya kuichukulia tahadhari, juu ya kuwa katika wanavyuoni wako wenye kusema kuhusiana na sala ya walio upande wetu (Ibadhi), kuwa hakika sala hiyo ni sahihi kwa makubaliano ya wote; kwa sababu waliyoyaacha katika matendo ndani yake ni yenye mizozano ndani yake kwa wengine, na mwenye kuyakubali haoni kuwa kuachwa kwake hayo kunapelekea kubatilika kwa sala...)) [Al-Allaamah Ahmed Al-Khalili Al-Afatawa 1/253]
Kwa upande wa Ibadhi, hakuna khilafu katika safu zao kuhusiana na suala hili kuwa haifai kunyanyua wala kufunga mikono katika sala.Ya ajabu katika suala hili:
  1. Ni kuwaona wenye kulithibitisha wanalishadidia sana bila ya hoja wala dalili ya kubatilika sala ya asiyelifanyia kazi.
  1. Ni kuwaona wenye kulithibitisha wanatofautiana katika suala hili na kila mmoja anaona dalili zake ndio sahihi na za wengine ni dhaifu basi:
  1. Hanafi wao wanaona kufungwa mikono chini ya kitovu, nao wana hoja zao na kudhoofisha hoja za wengine.
  1. Maliki wao wanaona kunyanyua mikono tu wakati wa kuhirimia kisha kuirejesha katika hali yake kama ilivyokuwa, nao wana hoja zao na kudhoofisha hoja za wengine.
  1. Shaafii wao wanaona kufunga mikono juu ya tumbo karibu ya kifua, nao wana hoja zao na kudhoofisha hoja za wengine.
  1. Hambali wao wanaona kufunga mikono ni juu ya kifua karibu na shingo, nao wana hoja zao na kudhoofisha hoja za wengine.
  1. Makubaliano yamepita kuwa Mtume (s.a.w) amesema: ((Salini kama munavyoniona ninasali)) na matendo haya ni katika matendo ya dhahiri; basi vipi yawe na khilafu na mizozo ndani yake?!
Hayo yote yanaonesha udhaifu wa suala hili katika sala bila ya shaka yoyote ile; hasa hasa tukizingatia kuwa kila wana madhehebu wanadhoofisha hoja za wengine kidalili na wote wanakusanyika katika chuo kimoja cha Ahalu Sunna wal-Jamaa.Tukirudia katika Hadithi zilizopokewa katika suala hili tunazikutia si katika sahihi kiuhakikisho, kwani yenye nguvu zaidi katika hizo ni Hadithi moja aliyoipokea Bukhari katika suala la kufunga mikono, nayo haina bayana ya kuwa inatoka kwa Mtume (s.a.w), imekuja ndani yake: ((Walikuwa watu wakiamrishwa, mtu aweke mkono wake wa kulia juu ya dhiraa yake ya kushoto katika sala)) [Bukhari 740] nani akiamrisha na wakati gani?!!!Hadithi hii:
  1. Imepita kwa Malik bin Anas, naye ndiye Imamu wa Madhehebu ya Malik, Imam Malik hakuifanyia kazi Hadithi hii, hivi wao wanaweza kumtuhumu Imam Malik kutofanyia kazi Sunna ya Mtume (s.a.w).
  1. Ina utata ndani yake; kwani Bukhari ameipokea hadithi hii kupitia kwa Mashekhe wake wawili nao ni Abdullahi bin Maslamah na Ismail bin Abi Uwais ambao wameipokea kutoka kwa Imam Malik na yeye kutoka kwa Abu Hazim, Masheikh hawa wa Bukhari wametofautina:
  1. Abdullahi bin Maslamah anasema kuwa Abu Hazim kasema: Silijui hilo isipokuwa analiegemeza kwa Nabii (s.a.w).
  1. Ismail bin Abi Uwais anasema: "hapana Abu Hazim hakusema hivyo, bali alisema kuwa linaegemezwa hilo kwa Mtume (s.a.w)".
Inaonesha kuwa Sheikh Abdullahi bin Maslamah alitaka kumsemea Abu Hazim kuwa kasema Sahaba Sahal bin Saad ndiye aliyeliegemeza hilo kwa Mtume (s.a.w) na kuwa ndiye aliyekuwa akiamrisha watu, lakini Shekh Ismail akakataa hilo na kulidiriki kwa kusema kuwa Abu Hazim alisema kuwa hilo lilikuwa linaegemezwa kwa Mtume (s.a.w); kwa hiyo ni nani aliyekuwa akiliegemeza?!!Riwaya ina utata, na riwaya yenye utata ni dhaifu.Sisi sote tunajuwa, kuwa baada ya kuanguka kwa Dola ya Khalifa wa nne Aliy bin Abi Twalib (k.a.w) ulifuatia utawala wa kimabavu wa Muawiyah bin Abi Sufiayan ambaye makao makuu yake yalikuwa Shaam katika mji wa Damaskas katika nchi ya Siyria, na tunafahamu kuwa Shaam ndiyo kitovu cha Ahalu Al-Kitaabi (Mayahudi na Manasara), na sote tunafahamu kuwa mapokezi ya Hadithi yalichezewa na kupelekea hilo kuzuliwa Mtume (s.a.w) yasiyokuwa yake, na kwa hiyo ikaanza elimu ya kuchunguza Hadithi za Mtume (s.a.w); ili kuzijuwa ni zipi dhaifu na zipi sahihi, pia tunafahamu vizuri, vipi Masahaba na Matabiina walivyokuwa wakijitahidi katika kufanyia kazi Sunna ya Mtume wetu (s.a.w).Sasa tuangalie haya yafuatayo:
  1. Anatuambia Ibnu Rushd Al-Hafiid katika kitabu chake Sharhu Bidaayatu Al-Mujtahid wa Nihaayatu Al-Muqtasid 1/323 haya yafuatayo: ((Suala ya tano: Wametofautiana Maulamaa katika kuweka mikono miwili mmoja wao juu ya mwengine katika sala, basi akalichukia hilo Malik katika faridha na akalikubali katika nafila, na watu wengine wakaona kuwa kitendo hicho ni katika sunna za sala, nao ni jamuhuri. Na sababu ya kutofautiana kwao, ni kuwa zimekuja athari zilizothibiti imenakiliwa ndani yake sifa ya sala yake (s.a.w), na haikunakiliwa humo kuwa yeye alikuwa akiweka mkono wake wa kulia juu ya wa kushoto, na imethibiti pia kuwa watu walikuwa wakiamrishwa kwa hilo.....)) mwisho wa kunukuu.
  1. Anatuambia Abu Bakar Muhamad bin Ibarahim bin Mundhir Niisabuuri aliyefariki mwaka 318 HJ katika kitabu chake Al-Ishraafu 2/12: ((Na wameona jamaa kunyoosha mikono, na miongoni mwa tuliopokea hayo kuwa kwao ni: Ibnu Zubair, na Hassan Al-Basari, na Ibrahim Anakhaii)) mwisho wa kunukuu.
  1. Imekuja katika Twabaqaatu Al-Huffadhi cha Dhahabii 3/213 kuwa Abdurazaq amesema: ((Sijamuona aliyekuwa akisali vizuri kuliko Ibnu Juraij, amechukuwa kutoka kwa Ataa na amechukua Ataa kutoka kwa Ibnu Zubar, na amechukua Ibnu Zubair kutoka kwa Abu Bakar Siddiiq, na ameichukuwa Abu Bakar kutoka kwa Nabii (s.a.w)...)) na sisi tumeona hapo no. 2 kuwa Ibnu Zubair hakuwa akifunga mikono.
  1. Sheikh Al-Imam Mohammad Aaabid -Mufti wa Malik katika mji wa Makka katika zama zake- anatuambia katika kitabu chake Al-qaulu Al-faslu ukurasa wa 3: ((Nasema: tuhuma hii ni batili kwa njia tatu: Njia ya kwanza: Hakika kukamata mkono, hakujapokewa kwa njia sahihi hata moja isiyokuwa na maneno ya kusemwa ndani yake, isipokuwa kwa njia ya Sahal bin Saad aliyopokewa katika Muwatwaa na Bukhari na Muslim)) kisha kaileta hadithi hiyo ya Bukhari kisha akasema: ((Pamoja na kuwa usahihi wa sanadi yake hauna doa lolote sio mwanzo wala mwisho, isipokuwa Daanii amesema katika Atraafi Muwatwaa: "Hadithi hii ni maaluul; kwa sababu ni dhana kutokea kwa Abu Hazim kwa neno lake silijui hilo ..")).
  1. Imekuja katika kitabu cha Tarikhi Abi Zur-aa Damashqii riwaya no. 1785 (kutoka kwa Bakar bin Amru kuwa yeye hakuwahi kumuona Abu Umaamah -yaani mwana wa Sahal- akiweka mmoja wa mokono wake juu ya mwengine hata mara moja, wala (hakuwahi kumuona) yoyote katika watu wa Madina, mpaka alipofika Shaam ndio akamuona Auzaaii na watu wanaiweka).
  1. Amepokea Ibnu Abi Shaibah (mpokezi wa Kisunni) katika Musannaf 3/319 riwaya no. 3958 kuwa Mtume (s.a.w) amesema: ((Kama mimi nawaona wataalamu wa wana wa Israili wakiwa wanaweka mikono yao ya kulia juu ya mikono yao ya kushoto katika sala)).
Hebu tuangalie kwa jicho la uadilifu ndugu zangu, hivi inawezekana katika wakati huo wa Masahaba na Matabiina kuwa sunna ya kufunga mikono katika sala haijulikani katika mji aliokufa ndani yake Mtume wetu (s.a.w), kisha sunna hiyo inafanyiwa kazi Shaam (ambako ndio makazi hasa ya Ahalu Al-kitaabi) kwa Muawiyah?! Kisha sunna hiyo ikaingiwa na utata wa kila rangi ndani yake?Ndugu zangu, sio ajabu kwa Ibadhi kutofunga mikono katika sala; kwa sababu wao wakati huo ndio waliokuwa waislamu wa Oman ambao waliusihi uislamu tokea mwaka wa sita Hijiria kabla ya kufa Mtume wetu (s.a.w) kwa miaka minne, tena kwa hiyari zao, na hawakukubali kuathirika na fitna zilizotokea katika zama hizo, na kwa hiyo walikuwa mbali na athari zake, bali la ajabu ni kusemwa Ibadhi eti wanapingana na Sunna ya Mtume (s.a.w), hali ya kuwa kiuhakikisho si Sunna ya Mtume (s.a.w) bali ni penyezo la malengo ya kisiasa la kuwajuwa ni nani waliokuwa katika safu za Muawiya na wenzake na nani wako katika asili ya wema waliotangulia (r.a)?.Tukirudia tena, tunasema kiasili Muislamu anaposimama katika sala huwa hafungi mikono; kwa hiyo kutofunga mikono katika sala hakuhitaji dalili aslan, isipokuwa dalili ya kukusanya, kama vile kuhakikisha unyenyekevu katika sala ambako kunalazimisha kutofanya harakati yoyote ndani yake, kwa hiyo mwenye kuja na tendo la ziada ndiye anayetakiwa athibitishe madai yake.Na kwa kumalizia kidalili, tunasema kuwa Mtume (s.a.w) amekataza kunyanyua mikono katika Sala katazo la ujumla, kwa hiyo linakusanya kukatazwa kila harakati za kunyanyua mikono katika sala, ikiwa ni kiunyanyua, au kuifunga, au kutikisa kitu katika hiyo mikono kwa kukinyanyua kwa makusudi, ikiwa ni kidole au chenginecho.Anatuambia Mtume wetu (s.a.w): ((Vipi mimi ninakuoneni kunanyanyua mikono yenu kama kwamba ni mikia ya farasi wakaidi?! Tulizaneni katika sala)) [Muslim 430 Ahmed 20875 Abu Daudi 823]Kwa hiyo Ibadhi wapo katika kutekeleza fundisho la Mtume (s.a.w) la kutulizana katika Sala, basi sisi ni wenye kutulizana kama alivyotufundisha Mtume (s.a.w), sala yetu haina harakati yoyote ya kuvunja utulivu ndani yake.

Post a Comment

No comments