*Fatwa za Mstahiwa Sheikh Ahmed Al Khaliliy.*
_(Muft Mkuu wa Oman.)_
_Mfasiri: Sheikh Munir Al Masroury._
*KUMWINGILIA MKE KWENYE NJIA YA NYUMA.*
➖➖➖➖➖➖➖➖➖
*SUALI:*
Ni miongoni mwa yanayojulikana kuwa mwenye kumwingilia mkewe kwenye njia ya nyuma humharamikia mkewe uharamu wa milele. Lakini aliyetenda tendo hili baya akiwa hayajui haya halafu akajua uharamu wa tendo hili, nini hukumu katika hali hio?
*JAWABU:*
Uharamishwaji milele wa mke aliyeingiliwa na mumewe katika njia ya nyuma hauna msingi wa dalili ya kisharia zaidi ya ’al-iya'la’ waliyoitegemea baadhi ya wanazuoni wa Fiqhi, ambayo ni kuiziba milango ya uovu na kuzifunga njia zake kwa waovu, nalo ni jambo zuri kama lisingeleta matatizo ambayo ufumbuzi wake hatuna. Kwani kumharamisha mke huyo kwa mumewe kutapelekea kumhalalisha kwa mwengine; na maadamu akdi ya ndoa yao
imethibiti kwa andiko la kisharia basi na utenganisho
utakaomhalalisha kwa mwengine hauna budi nao uwe umethibiti kwa andiko la kisharia; Vinginevyo nini kinachomhalalisha kwa mwengine?
Kwa ajili hiyo mimi naona kuwa toba inamtosheleza kuhusiana na jambo hilo; maana suala hili ni hatari. Na Mwenyezi Mungu Ndiye wa kuombwa auni na Ndiye Mjuzi zaidi wa lilo sawa.
*SUALI:*
Nini hukumu ya kumwingilia mke mdomoni na kwenye njia ya nyuma na katika hedhi? Na nini kinamlazimu mwenye kufanya hayo?
*JAWABU:*
Kumwingilia mke mdomoni bila Shaka ni kinyume na maumbile, lakini haikuja dalili ya maandiko kutoka kwa Mwenyezi Mungu au Mtume Wake kuhusu hukumu ya hilo; isipokuwa hapana Shaka kwamba mdomo ni sehemu inayopasa kutakaswa. Kwani mdomo kwa upande mmoja ni pa kuingilia chakula na kinywaji, na kwa upande mwengine ni sehemu ya kutajwa Mwenyezi Mungu, na kwa hiyo ni lazima isichafuliwe kwa uchafu wowote. Na ni katika yanayojulikana kwamba kuingiza uume kinywani katika wakati huo kama hapajatoka manii huenda kukapelekea kutoka aina nyenginezo za majirnaji zikaingia mdomoni; na majimaji haya yote unajisi wake hauna shaka. Kwa ajili hiyo tunasema jambo hili ni haramu, lakini hatusemi kuwa linawajibisha kitu. Ama kumwingilia mke wakati wa hedhi, yamekuja mapokezi kadha yanayokubaliana kuwa hilo, pamoja na kuwajibisha kutubu kwa Mwenyezi Mungu mtakatifu aliyetukuka, huwajibisha pia kufanya kafara, ambayo huitwa dinari ya tandiko, yaani mtu agawe thamani ya dinari ya dhahabu kwa mafakiri na maskini. Na likapimwa na hilo katika hukumu ya kafara suala la kumwingilia mke kwenye njia ya nyuma kwa vile mawili yote ni haramu.
*Na Allah anajua zaidi.*
➖➖➖➖➖➖➖➖➖
No comments