Header Ads

Cup of coffee on saucer

HII NDO BIDAA YA MAULIDI BOFYA KUFAHAM ZAIDI


Mawlid Ni Bid'ah Na Vigawanyo Vya Bid'ah Pia Ni Bid'ah


Sulaymaan Muhammad ‘Abdur-Rahmaan




Maulidi ni Bid’ah, wanachuoni wote wamekubaliana hili hata wale wanaounga mkono Maulidi. Tofauti yao ni kwamba, hii ni Bid’ah njema.

Hivyo ili kujua uhakika wa Maulidi, itabidi ufahamu nini hukumu ya Bid’ah.

Mimi naanza kuzungumzia Bid’ah.

Kuhusu bid’ah, wanachuoni wamegawika sehemu mbili,

1.     Kundi la kwanza ni lile linalosema Bid’ah ni aina mbili, mzuri na mbaya. Katika kundi hili wapo walioenda mbali zaidi wakasema Bid’ah ina sehemu tano:

a.     Bid’ah ya Waajib

b.     Bid’ah ya Sunnah

c.      Bid’ah ya Mubaah

d.     Bid’ah ya Makruuh

e.     Bid’ah ya Haraam


Tukianza na kundi hili na wanachuoni waliopita katika mtazamo huu.

a.     Imaam ash-Shaafi’iy.  Yeye amesema Bid’ah ni aina 2. Bid’ah nzuri na mbaya. Akafafanua, akasema, Bid’ah nzuri ni ile inayowafiki Qur-aan na Sunnah. Ama Bid’ah inayokhalifu Qur-aan na Sunnah hiyo ni mbaya.

b.     ‘Izzud-Diyn bin ‘Abdis Salaam (amekufa mwaka 660 Hijriya)

Yeye ndiye ndiye aliyegawa Bid’ah katika sehemu 5 katika kitabu chake cha Qawa’id juzu ya 2, ukurasa 337 hadi 339.

Tanbihi:

Maulamaa wote wanaogawa Bid’ah katika makundi mawili ama 5 ama idadi yoyote ile, rejea yao kubwa ni maimaam hawa wawili, aidha
Imaam ash-Shaafi’iy ama ‘Izzud-Diyn, miongoni mwa hao ni:

  1. Imaam Abuu Shamaa, Shaykh wake Imaam an-Nawawiy

  1. Imaam an-Nawawiy katika kitabu chake cha Tahdhibul-Asmaa


  1. Imaam al-Bayhaqiy

  1. Ibn Hajar al-Haytham na wengineo.



2.     Kundi la pili la wanachuoni ni lile linalosema Bid’ah zote ni mbaya hazina kheri,


Kundi hili lina wanachuoni wengi sana kuanzia Imaam Maalik, Ahmad bin Hanbal, Ibnul Qayyim, na waliokuja baadaye.

Ama kubhusu hoja ya kugawa katika makundi mawili ama matano zimejibiwa kwa fasaha sana na Maulamaa wafuatao:

Kuhusu hoja ya Imaam ash-Shaafi’iy:

Ameileza Muhammad bin ‘Abdul-‘Aziyz katika kitabu chake cha Araau Ibn Hajar al-Haythamiy kwamba:

  1. Imaam ash-Shaafi’iy katika kitabu chake cha ar-Risaalah, amesema hivi, Mtu yeyote, ataye fanya kitu kizuri, huyo ameifanya shari’ah, na haitakiwi kuifanya shari’ah mtu yeyete ila Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Hivyo kauli yake hii inapingana na ile ya kuigawa Bid’ah.

  1. Namna ya pili, kuhusu hoja ya Imaam ash-Shaafi’iy, ameileza Ibn Rajab katika Jaami’ Uluum, kuwa muradi wa ash-Shaafi’iy, kusema bid’ah nzuri ni Bid’ah kwa maana ya kilugha na si kwa maana ya kishari’ah.

Ama kuhusu kuzigawa katika sehemu tano, Imaam ash-Shaatwibiy (amefariki mwaka 690 Hijriyah), katika kitabu chake cha al-I’itswaam, amesema hivi:

“Kuzigawa bid’ah katika sehemu tano ni Bid’ah kwani hakutambuliwi na shari’ah.”
Akaendelea kwa kusema,
“Ikiwa Bid’ah itabidi iangukiye katika makundi hayo matano, basi ingekuwa hakuna Bid’ah, maana kitu ama kingekuwa Haraam, Sunnah, Mubaah, Makruuh, ama Haraam.”

Kwa hiyo akairudi kauli ya ‘Izzud-Diyn bin ‘Abdis-Salaam kwamba Bid’ah zote ni upotevu na kwamba, vitu vya Haraam vinajulikana, Sunnah, Mubaah na Makruuh na Haraam vyote vyajulikana. Mtu asiingize Bid’ah katika dini.


Hoja za kukataa kuzigawa Bid’ah zimeegema katika dalili zifuatazo:

1.     Dini imeshakamilika tangia kabla Mtume hajafariki, Qur-aan: 5: 3

2.     Mtume amesema Kullu bid’ayin dhwalaalah, (Hadiyth ya 28 katika 40 an-Nawawiy-amepokea at-Tirmidhiy) hajagawa Bid’ah.

3.      Mwenye kuzua jambo katika dini yetu hii, ama mwenye kufanya ‘amali ambayo haikufata mafundisho yetu, kitarudishwa kitu hicho na hakikubaliwi (Hadiyth ya 5 katika 40 an-Nawawiy- Mutafaqun ‘alayhi).

4.     Imepokewa na Al-Bukhaariy 8084 na Muslim 1847 Hadiyth maarufu aliyoipokea Hudhayfah, ni ndefu, naomba niinukuu maana yake kadri Allaah Atavyoniwafikisha, ukitaka matni yake tembelea nambari hizo za Hadiyth hapo juu kwa al-Bukhaariy ni kitabu al-fitnah- babu al-Amr idhaa lamtakun jama’at, na kwa Muslim, kitabu al-Imaarat- babu wujuub mulaazamat jamaat al-Muslimiyn ‘inda dhuhuuri al-Fitnah. Nayo ni hii: Hudhayfah kasema, watu walikimuuliza Mtume mambo ya kheri lakini mimi nikimuuliza mambo ya shari nikichelea yakinikuta nichukue tahadhari, nikamuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) “Tulikuwa katika mambo ya ujinga na shari, Akatuokoa Allaah kwa kwa kutuletea kheri hii ya Uislam, je, baada ya kheri hii itakuja shari? Mtume akasema ndiyo, Hudhayfah akauliza, je, baada ya shari hiyo itakuja kheri, Mtume kasema ndiyo, lakini ina Dakhnu, nikamuuliza nini dakhnu, akasema “Ni watu wanafuata mwenendo ambao sio mwenendo wangu mimi na wanaongoza bila kufuata muongozo wangu mimi, kuna mambo utakubaliana nao lakini mengine hutoyakubali.” Hudhayfah akauliza, je, baada ya kheri hiyo kutakuwa na shari, akasema ndiyo, watu wanawaita watu hali yakuwa wamesimama katika milango ya Jahannam, atakayewafuata wanamtosa katika Jahannam, Hudhayfah akmwambia tupe sifa zao watu hao, Mtume akasema, “Ni watu kamasisi na wanatamka kwa Maneno yetu.” Hudhayfah akasema unanishauri nini ewe Mtume ikiinikuta hali hiyo? Mtume akasema, “Jilazimishe kuwa katika jamii ya Waislam na kiongozi wao, Hudhayfah, akauliza, ikiwa hakuna mjumuiko wa Waislam wala kiongozi, (bali kuna makundi makundi mengi) Mtume akamwambia “Achana na makundi hayo yote, ni bora kwako kuenda kung’ang’ania shina la mti na umauti ukukute hapo”. Hii ni tahadhari aliyoitoa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

5.     Mtume amesema “Sijaacha kitu chochote kile kitacho kukurubisheni ingiza peponi ila nimekujulisheni na pia sijaacha kitu chochote kile kitachokuwekeni mbali na moto ila nimekujulisheni.” (Musannaf ‘Abdur-Razaaq, Hadiyth ya 20100 juzuu ya 11 ukurasa wa 125). Kama Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ameshatufundisha kila cha kutupeleka peponi na kila cha kutuepusha na moto, tuna haja gani ya kuwa na Bid’ah.

6.     Mtume anasema Hadiyth ameipokea Imaam Muslim,“Hakuna Mtume yeyote aliyepelekwa na Allaah kabla yangu mimi ila alikuwa na wafuasi (Maswahaba na walinzi wa I’itiqaad) wanachukua mwenendo wake na wanaufuata mwenendo wa Mtume huyo, kisha wanakuja watu baadaye wanakhalifu, wanasema wasiyo yafanya, na wanafanya wasio amrishwa, mwenye kupambana nao kwa ulimi ni Muumin, mwenye kupambana nao kwa ulimi pia ni Muumin, na zaidi ya hapo hakuna imani hata chembe ya khardali” (Muslim kitabu al-Iymaan- babu kawn nahyi ‘anil munkar minal Iymaan - Hadiyth ya 50).

7.     Hadiyth imepokewa na Imaam Muslim Mtume kasema:“Hakupeleka Allaah Mtume, ila ni haki ya Mtume huyo kuwajulisha umati wake kheri anayoijua Mtume huyo kwa umati wake huo, na pia kuwajulisha shari anayoijua.” (Muslim - kitabu l’imarat-bau wujubu lwafaau bibay’ lkhulafa - Hadiyth ya 1844). Ikiwa Mtume amesema hivi maana yake ni kwamba kila kitu cha kheri ametujulisha na cha shari ametujulisha, ya nini kuzua Bid’ah? Rejea namba 5 hapo juu. Na kwa hili, Imaam Maalik amesema, “Yeyote atakayezua jambo katika dini na akasema ni bid’ah hasanah huyo anamzulia Mtume kwamba hakufikisha hiyo kheri na yeye ameivumbua.”

8.     Ibn Mas’uud amesema, siku moja Mtume alichora mstari ulonyooka, kasha akaweka matawi kuelekea pande mbalimbali. Kisha Mtume akasema huku akionesha ule mstari ulionyoka (Akasoma: “Wa Anna haadha swiratwil Mustaqiym.” Surah ya 6: 153 Suratul An’aam), kisha akavionesha vijia vidogovidogo akasema wala tatabi’u subula.. muendelezo wa Aayah hiyohiyo.

9.     Ibn Mas’uud huyu, aliletewa khabari na Abu Muusa kwamba kuna msikiti fulani, watu wakati wanaisubiri Swalah, kuna mambo ya ajabu wanafanya. Akamwabia twende tukawaone, akaenda Ibn Mas’uud, alipofika pale, akawakuta watu wamezunguka duara, na wana vijiwe, kisha mmoja wao asema “Semeni La ilaaha illa Allaah mara 100 ( Halliluu mia) wale watu wanasema (La ilaaha illa Allaah), semeni takbira mia, n.k. Ibn Mas’uud akawambia, nini hii, wakasema tunakusudia kheri. Ibn Mas’uud akasema, aidha ninyi mna dini mzuri kuliko ya Muhammad au ni wazushi, na kamamwakusuida kheri, wangapi wamekusdia kheri na wameikosa. Ibn Mas’ud akakemea Bid’ah ile. Hao ndo Maswahaba walivyokuwa hawakubali uzushi.

10.             Kuhusu wanachuoni kuigawa Bid’ah, Shaykh Ibn ‘Uthamiyn amemnukuu Ibn ‘Abbaas akisema, “Nyinyi vipi mimi nawaambia Mtume amesema hivi nyinyi mwaniambia Abu Bakr, ‘Umar, nakhofu kuteremka Mbinguni mawe juu yenu, ninyi mnayabeza maneno ya Mtume kwa Abu Bakr, ‘Umar.” Huyo ndiye Ibn ‘Abbaas, akikemea mtu kupinga kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

11.             Hudhayfah, Swahaba wa Mtume, amesema, “Enyi wasomi, fuateni Qur-aan na Sunnah mtakuwa na msimamo thabiti, wala msizue mtaharibikiwa.” (Al-Bukhaariy)

12.             MaImaam wote wanne wamesema wazi, ikiwa imethibiti Hadiyth sahihi ya Mtume, ikawa inapingana na kauli yake, kauli yake itupwe na wala isiwe hoja. Na hiyo kauli ya Mtume ndio madh-hab yake. (Abu Haniyfah, Maalik, ash-Shaafi’iy, Hanbal. Thawriy).

13.             Imaam Maalik amesema, Maneno ya mtu yeyote katika dini hii, huchukuliwa na hutupwa ila kauli ya bwana mwenye kaburi hili (akionesha kaburi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)).

14.             Na Aayah nyingi za Qur-aan (An-Nuur: 63, Al-Hashr: 7, Al-Maaidah: 3, Ash-Shuuraa: 21) Aayah hizi zote ukizosoma kwa makini na mufasirina wote wanaokubalika, wamethibitisha zinapinga Bid’ah katika dini. Rejea Ibn Kathiyr.


Kwa ufupi hizo ndizo hoja bayana za kupinga Bid’ah na kwamba hakuna bid’atun hasanah.

Kama hivyo ndivyo na kwa kuwa Maulidi ni Bid’ah, basi Maulidi ni Bid’ah ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema Kullu bid’atin dhwalaalah, hayana kheri.

Hili ni jawabu la jumla.


Ama hoja ya kuwa Maulidi yanafaa kuhusu kisa cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwakuta mayahudi wanafunga siku ya ‘Aashuraa, alipowauliza wakasema ni kuadhimisha siku aliyookolewa Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam).

Hii ni hoja ambayo Ibn Hajar al-‘Asqalaaniy ndiyo aliyoitumia kujuzisha Maulidi na kusema hivi katka fatwa yake “Maulid ni Bid’ah kwani hawakufanya Salafus Swaalih, lakini kwa yale mazuri yanayopatikana, kufanya takrima, kumdhukuri Allaah n.k. basi ni Bid’ah nzuri”

Kwa maelezo haya, Ibn Hajar, na mwanafunzi wake Imaam as-Sakhaawiy, wamesema Maulid ni bid’atun hasanah.

Hoja hii imejibiwa kama ifuatavyo:

1.     Kwa kuwa Ibn Hajar, amekiri ni Bid’ah na wala Salafus Swaalih hawakufanya, basi haiwezi kuwa hoja, na lau angerejea malezo ya Imaam ash-Shaatwibiy (kamatulivyoeleza huko juu ya kupinga kugawa Bid’ah) basi asingesema hayo. Hivyo kauli yake hii inatupwa. Tazama haya katika kitabu “Qawlul Faswil fiy Hukmih Ikhtifaal bi Mawlid khayri Rusli” (Mwandishi –Ismaa’iyl bin Muhamad al-Answaar).

2.     Namna ya pili ni kwamba, funga ya ‘Arafah amefundisha Mtume na Maulidi ni Bid’ah, hakufundisha.

3.     Mtume ameadhimisha, siku aliyozaliwa kwa kufunga, hivyo anayetaka kumuadhimisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa kushereheka siku aliyozaliwa, basi na afunge, ndicho alichofundisha.

4.     Qiyaas hakitumiki kuvumbua ibada.

5.     Ibada inahitaji dalili.


Hoja yao Nyingine kuhusu Maulidi yanafaa kuhusu kisa cha Abuu Lahabi,

Majibu ni kama ifuatavyo:

1.     Hadiyth ya kisa hiki ni dhaifu (Mursal) na kwamba Abuu Lahabi hakumuacha huru Thuwaybah siku ile alompelekea khabari ya kuzaliwa Mtume. Ukweli ni kuwa Abuu Lahabi alimuacha huru, muda mrefu mpaka Mtume alopokuwa amehamia Madiynah. Tazama, Fat-hul Baariy ya Ibn Hajar- kitabu Radhaa.

2.     Pia Ibn Hajar asema, inapingana na Aayah iliyopo katika Suratul Furqaan 25: 23 isemayo, mambo mema yote walofanya makafiri hapa duniani yatakuwa vumbi tu. Hivyo sio kisa sahihi.

3.     Ama kusema, hiyo, itakuwa ni sawa na kwa mzee Abuu Twaalib, wanachuoni wasema, kisa cha Abuu Tawalib kupunguziwa adhabu, imethibiti Hadiyth sahihi, lakini kisa cha Abuu Lahabi, hadithi si sahihi, na ni ndoto, na ma Hufaadh wameirudi.

Kwa maelezo haya,

Maulidi ni Bid’ah kwani hayajafundishswa na Mtume, na wala Salafus Swaalih. Ibada inahitaji dalili sio Qiyaas wala kubuni.

Mambo ya kheri yote Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ameyafundisha, iweje ipatikane khiri wakati Mtume ameshafariki?
Rejea dalili  namba 5, 7 hapo juu, utauona ukweli huu.

No comments