Kwa kuzingatia kwamba, wanawake wanaunda
nusu ya mwili wa jamii na wana nafasi muhimu katika kuleta na kueneza
haya, staha, usafi na maadili katika jamii ya mwanadamu, katika kipindi
chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 39 ya mfululizo huu, tutajadili
na kuzungumzia maudhui ya staha na haya kwa wanawake kama ilivyokuja
katika hadithi. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
*******
Staha na utakasifu ni jambo ambalo
limechanganyika na kuumbwa mwanamke. Imam Ja’afar Swadiq (a.s) anasema
kuhusiana na staha na haya kwamba: Haya ina vipengee kumi na vipengee
tisa kati ya hivyo kumi vinapatikana kwa wanawake na kipengee kimoja
kilichobakia kiko kwa wanaume..
Katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa
Bwana Mtume (saw) pia inasema: Haya ni jambo zuri, lakini kwa wanawake
ni jambo zuri zaidi.
Kwa hakika hadithi hizi zinabainisha
kwamba, sehemu kubwa ya masuuliya na majukumu ya kuhifadhi staha na
maadili katika jamii iko mikononi mwa wanawake. Kwa kuzingatia uhakika
huo, wanawake wastahiki wanapaswa kuwa makini zaidi kuliko wanaume
katika kuhifadhi hijab, namna ya kuzungumza na hata katika utembeaji
wao.
Tunaporejea katika Kitabu Kitukufu cha
Qur’ani tunapata kwamba, suala la haya kwa wanawake limeashiriwa kwa
njia mbalimbali. Katika aya ya 31 ya Surat Nur Mwenyezi Mungu
anabainisha kwamba, mwanamke mwenye haya na staha ni Yule anayejistiri
na kuchunga heshima, staha na hijabu yake kwa mtu asiye maharimu wake.
Aya hiyo inasema:
Na waambie Waumini wanawake wainamishe
macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa
unaodhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala
wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume
zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka
zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyowamiliki mikono
yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao
hawajajua mambo yaliyokhusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili
yajuulikane mapambo waliyo yaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu,
enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa.
Kwa msingi huo basi, ishara ya haya ni
wanawake kujistiri kikamilifu na hilo ni jambo ambalo limeashiriwa
katika aya iliyotangulia na wanawake wametakiwa kuiambatanisha pamoja
miamala yao na kuona haya na soni. Kutoonesha uzuri wao kwa watu wasio
maharimu kwao kwa wanawake waumini ni ishara na athari ya kuona haya na
kuwa staha wanawake.
*******
Mtume Muhammad (saw) anabainisha na
kutambulisha mavazi ya wanawake kwa wanaume ambao sio maharimu wao
kwamba, ni kigezo cha ubora wa mwanamke. Anasema: Wanawake wenu walio
wabora ni wanawake wenye staha, ambao hujipamba kwa ajili ya waume zao
tu, na hujistiri kikamilifu kwa wasiokuwa waume zao.
Siku moja Bwana Mtume (saw) alisema: Je
nikuambieni wanawake wabaya kabisa kwenu nyinyi ni wepi? Kisha akasema:
Wanawake wenu walio wabaya kabisa ni wale wanaojipamba mbele ya wengine
lakini mbele ya waume zao hujifunika na hawaoni ulazima wa kujipamba
mbele ya waume zao.
Katika Surat al-Qasas, Qur’ani tukufu
inabainisha sehemu ya maisha ya Nabii Mussa (a.s) na kisa cha kukutana
kwake na mabinti wa Nabii Shuaib (a.s). Mabinti ambao mwenendo na
muamala wao ulikuwa umejaa staha, haya na heshima. Kisa hicho kinaeleza
kuwa, wakati Nabii Mussa (a.s) alipo yafikia maji ya Madyana alikuta
umati wa watu wananywesha (wanyama wao), na akakuta karibu yao mabinti
wawili wanawazuia wanyama wao. Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi
sisi mpaka wamalize hao wachunga. Na baba yetu ni mzee sana. Basi Nabii
Mussa akawanyweshea. Baada ya mabinti wale kurejea kwa baba yao yaani
Nabii Shuaib (a.s) walimhadithia kuhusiana na msaada waliopewa na bwana
yule pamoja na upole na huruma aliyokuwa nayo kwao.
Nabii Shuaib (a.s) akamtuma mmoja wa
mabinti zake kwa Nabii Mussa ili akamualike nyumbani. Binti Yule
alikwenda mpaka alipo Nabii Mussa (a.s) na akampa habari kwamba, baba
yake anamuita.
Qur’ani Tukufu inabainisha jinsi binti
Yule alivyokuwa akimuendea Nabii Mussa na suala la haya, soni na staha
aliyokuwa nayo kwa kusema:
Basi mmoja katika wale wanawake wawili akamjia, naye anaona haya. Akasema: Baba yangu anakwita akulipe ujira wa kutunyweshea.
Hatua ya Qur’ani Tukufu ya kubainisha
mwenendo na mabinti wa Nabii Shuaib (a.s) ni sisitizo juu ya nukta hii
kwamba, kwa mtazamo wa Qur’ani, kuona haya na kuwa na staha ni miongoni
mwa sifa muhimu na za ukamilifu wa mwanamke. Binti ya Nabii Shuaib
sambamba na kuchunga, haya na staha alifikisha ujumbe kwa kutumia maneno
machache kabisa na bila kusema maneno ya pembeni na kumjulisha Nabii
Mussa juu ya wito wa baba yake na sababu ya mwaliko huo pale aliposema:
Baba yangu anakwita akulipe ujira wa kutunyweshea.
*******
Kwa hakika mwenendo na muamala wa
wanawake na wanaume katika jamii ni jambo lenye umuhimu mkubwa mno. Kuwa
na haya katika maneno na katika uzungumzaji ni jambo linalosisitizwa na
Mwenyezi Mungu pale alipowahutubu wakeze Mtume (saw) pale aliposema:
Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama
yeyote katika wanawake wengine. Kama mnamcha Mungu basi msiregeze sauti
zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake. Na semeni maneno
mema.
Pamoja na kuwa aya hiyo inawahutubu moja
kwa moja wake za Mtume (saw), lakini hukumu na amri hiyo haiwahusu
wakeze Mtume pekee, bali inawahusu wanawake wote wa Kiislamu. Kwa hakika
haya na soni inalazimu kwamba, uzungumzaji uwe kwa namna ambayo
itachochea na kumtia ushawishi mwanaume ambaye si maharimu kwa mwanamke.
Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana mafaqihi na Marajii wa dini
wanasema kuwa, kuzungumza mwanamke na mwanaume ambaye si maharimu wake,
au kuzungumza mwanamke huyo kwa namna ambayo sauti yake itakuwa ni ya
kuchochea hisia za matamanio za mwanaume huyo ni haramu.
Jambo jingine linalokatazwa ni mwanaume
na mwanamke ambao si maharimu kufanya mzaha usio na maana. Inaelezwa
kuwa, kufanya mzaha mwanaume na mwanamke ni jambo ambalo linawaweka
mbali na staha na haya.
Abu Basir anasimulia kwa kusema kuwa:
Nilikuwa katika msikiti wa Kufa
nikimfundisha Qur’ani mwanamke mmoja. Ghafla moja nikawa nimefanya naye
mzaha na utani. Ukapita muda, kisha siku moja nikapata fursa ya
kumtembelea Imam Muhammad Baqir (a.s) mjini Madina. Imam akanilaumu kwa
kitendo changu kile. Niliona haya na kuinamisha kichwa changu chini.
Imam Baqir (a.s) akasema: Fanya toba, na usifanye tena utani na mzaha na
mwanamke ambaye si maharimu.
Bibi Fatima Zahra (a.s) ni mfano kamili
wa mwanamke wa Kiislamu aliyekamilika katika kila sifa na aliyejipambana
kwa kila ukamilifu. Bibi Fatima alilipa kipaumbele suala la haya na
staha.
Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa kisa kifuatacho:
Siku moja Bibi Fatima alikuwa amekaa
pamoja na Bwana Mtume (saw), mara Bwana mmoja kipofu akabisha hodi na
kuomba idhini ya kuingia. Mtume (saw) akamuona Fatima amesimama na
kujistihi kwa hijabu. Mtume (saw) akasema, ewe binti yangu, bwana huyu
ni kipofu. Bibi Fatima akamjibu baba yake kwa kumwambia: Baba yangu
kipenzi, pamoja na kuwa yeye hanioni, lakini mimi ninamuona na ananusu
harufu ya mwanamke. Baada ya Mtume (saw) kusikia maneno yale, akasema:
Ninashuhudia kwamba, wewe ni pande la nyama yangu.
Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa tukutane tena wiki ijayo.
No comments