Header Ads

Cup of coffee on saucer

FADHILA NA UMUHIMU WA KUFUNGA SITA

Mountain View FADHILA NA UMUHIMU WA KUFUNGA SITA 4. Mlango wa kuhimiza kufunga Sita ya mfungo Mosi (Shawwal) 1. Imepokewa kutoka kwa Abu Ayyub رضي الله عنه akisema: Amesema Mtume ﷺ : “Atakayefunga Mwezi wa Ramadhani, kisha akaufuatilizia kwa kufunga siku sita katika mwezi wa Shawwal (Mfungo Mosi) atakuwa sawa na aliyefunga Dahari nzima.” (Dahari = Daima dawamu, Abadi) Imepokewa na Muslim, Abu Daud,Tirmidhi, Nasai, Ibn Majah na Tabarani. 2 . Imepokewa kutoka kwa Thawbaan, رضي الله عنه , Mwambata wa Mtume ﷺ akisema: Amesema Mtume ﷺ : “Atakayefunga Siku Sita, baada ya kufungua siku Kuu ya mwanzo (al-Fitr) atakuwa ametimiza kufunga mwaka mmoja (kisha akasoma Aya isemayo): “Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi.” (al-An’aam, 3: 160) Imepokewa na Ibn Majah na Nasai. Riwaya ya Nasa’i, inaongeza kusema: “…..Amejaalia Mwenyezi Mungu, kuwa Jema moja malipo yake ni mfano wake mara kumi; hivyo funga ya Mwezi mmoja wa Ramadhani ni sawa na funga ya miezi kumi. Na funga ya siku sita za Shawwali, baada ya Siku Kuu ya mwanzo, inakamilisha idadi ya kufunga mwaka mmoja.” 3. Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayra رضي الله عنه akisema: Amesema Mtume ﷺ : “Ataye funga Ramadhani, akafuatiliza kwa (kufunga) siku Sita katika Shawwal, atakuwa sawa na aliyefunga Dahari nzima.” Ameipokea al-Bazzar (Targhib wa Tarhiib: 3\1492) 4. Imepokewa kutoka kwa Abdullah bin Umar رضي الله عنهما akisema: Amesema Mtume ﷺ : “Ataye funga Ramadhani, akafuatiliza kwa (kufunga) Sita katika Shawwal, atatokana\atatasika na madhambi yake awe (hana dhambi hata moja) kama siku aliyozaliwa na mama yake mzazi.” Ameipokea Tabarani katika kitabu chake al-Awaswat, uk.8617 (Targhib wa Tarhiib: 4\1493) UFAFANUZI Funga ya Sita ni miongoni mwa Sunna kubwa sana, kama zinavyo ashiria Hadithi zote za hapo juu. Ni Sunna ambayo Mtume ﷺ ameisisitiza kwa kauli na vitendo. Ni Sunna ambayo, kama Hadithi zinavyosema na kuashiria, ni kikamilisho cha kukufanya kama umefunga miezi 12, yaani mwaka mzima; na hivyo kwa wale wenye kudumisha funga hiyo, baada ya kufunga kikamilifu Mwezi mzima wa Ramadhani, huwa na thawabu za kufunga maisha yake ya utuuzimani. Maana kila mwaka, akifunga Ramadhani moja, hupata thawabu za kufunga miezi kumi, na akikamilisha kufunga siku Sita katika mwezi wa Shawwali, baada ya Sikukuu ya mwanzo –maana ni haramu kufunga siku hiyo- basi anapata thawabu za kufunga miezi mwili mengine. Hivyo, amekamilisha kupata thawabu za kufunga mwaka mzima. Akifanya hivyo kila mawka, basi ni sawa na aliyefunga daima dawamu, milele katika maisha yake. Vile vile, ni Sunna kuzifunga siku hizo sita, kwa mtindo wa kufululiza -kama alivyokuwa akifanya Mtum ﷺ -, mara tu baada ya kumaliza kula Siku Kuu ya mwanzo, ya Iid al-Fitr. Kwani ni haramu kufunga Siku Kuu ya mwanzo ya Iid al-Fitr na Iid al-Adhha, vile vile. Hata hivyo, hapana ubaya iwapo atakatiza mtu, mfululizo huo; ilimradi Siku Sita hizo ziwe zimefungwa NDANI YA MFUNGO MOSI, kama zinavyo weza kueleweka Hadithi zote, ambazo zinasema: Akafuatisha Siku Sita KATIKA mwezi wa Shawwal. Baadhi ya Hadithi zimezungumzia: “Sawa na aliyefunga DAHARI” na neno Dahari linamaanisha: Daima dawamu, Milele, Abadi, Maisha na kadhalika. Hivyo, baadhi ya wanazuoni wameifasiri hivyo hivyo; kuwa ni sawa na aliyefunga Abadi. Na hawajakosea, hata kidogo. Kwani, mwenye kujiwekea utaratibu wa kufanya hivyo, mwaka hadi mwaka, basi huwa anapata thawabu za kufunga mwaka mzima kila mwaka, na ikiwa huo ndio mtindo wake- kama zinavyo ashiria Hadithi zote- basi ni sawa na mtu aliyefunga mwaka mzima, kila mwaka. Na hivyo, anakuwa ni mtu aliyefunga daima, dawamu, milele katika maisha yake. Hadithi nyengine, zinasema: “Sawa na aliyefunga mwaka mzima.”; maana ndiyo hiyo hiyo, yaani ukimaliza kufunga Ramadhani moja kisha ukafuatiliza kwa kufunga siku sita katika mwezi wa Shawwali, basi ni sawa na kufunga mwaka mzima. Hivyo, ukifunga mwaka huu na mwaka mwengine na mwaka mwengine, kwa mtidno wa kujiwekea kawaida, basi ni kama uliyefunga maisha yako yote ya ukubwani. Hadithi ya Nasai, inabainisha wazi wazi kuwa, vipi malipo hayo yanapatikana hivyo. Inasema ni kutokana na Malipo ya Jema Moja kwa malipo ya Mema Kumi= Ramadhani moja ni Ramadhani 10, na Siku sita ni mezi mwili. Hivyo, ni thawabu za kufunga mwaka mzima. Hivyo, atayefunga mwezi mzima wa Ramadhani atakuwa amefunga sawa na aliyefunga miezi kumi. Na akifuatiliza kwa siku sita katika mfungo Mosi, basi atakuwa sawa na aliyefunga siku 60 nyengine, ziada, na hiyo ni swan a miezi miwili, mengine. Kwa hivyo, atakuwa sawa na aliyefunga mwaka mzima. NASEMA: Yote hayo si makubwa kwa Mwenyezi Mungu! Mwenyezi Mungu Hashindwi - HASHA WA KALLA- kumlipa mja wake aliyefunga LILLAHI mwezi wa Ramadhani, kwa kumuamini kwa dhati Mwenyezi Mungu, na kutaraji Rehema Zake, kisha akafuatiliza kufunga siku sita katika Mfungo mosi - iwe kwa kufululiza baada ya Siku Kuu ya mwanzo, au kwa kukatiza – ilimradi ndani ya Mfungo mosi- HASHINDWI KUMLIPA thawabu za mtuu aliyefunga milele, sembuse mwaka mmoja. Na hii, ndiyo maana halisi ya Ahadi ya Mwenyezi Mungu, kwamba Swaumu ni Ibada yangu, na MIMI Ndiye mlipaji: الصوم لى وأنا أجزى به! Mwenyezi Mungu Amesema katika Hadith al-Qudsi, maarufu na mashuhuri sana, kuwa: “….Lau kama mngelikusanyika nyote, walio- kutangulieni na wajao, KATIKA UWANDA MMOJA, kasha kila mmoja wenu akaniomba atakalo, na Mimi nikampa kila aliyeniomba yale yote ambayo ameniomba, basi hapana kitachopunguza kitu kutoka katika Hazina yangu, zaidi ya kitacho weza tolewa na sindano iliyo chovywa kwenye bahari na kuopolewa” Muttafaq Alayhi. جل جلاله Ametukuka Kikomo cha Kutukuka, na Kutakasika kikomo cha Utakaso! Mwenye utajiri uso mipaka, wala kikomo, wala kuweza kukadiriwa na kukisiwa na kiumbe yeyote. YALIYOMO NA YATOKANAYO 1. Swaumu ya Sita ni Sunna ya kauli na vitendo. Mtume ﷺ amefunga na kuhimiza Waumini wafunge. 2. Fadhila za kufunga Sita ni nyingi na kubwa mno. 3. Swaumu ya Sita ni kama zawadi nyongeza kwa waliofunga Ramadhani kamili. (Zaka ya Fitri ni kitakaso cha Swamu na Swaumu ya Sita ni tunzo ya Swaumu ya Ramadhani) 4. Swaumu ya Sita inaweza kufungwa kwa mfululizo, iwe mwanzoni, katikati au mwisho wa Shawwal, kama inavyo juzu, vile vile, kufunga kwa kukatisha katisha: ilimradi siku zote ziwe zimefungwa ndani ya Shawwal. 5. Thawabu za funga ya mwaka mzima, hazipatikani isipokuwa kwa kufunga, kwanza, mwezi mzima wa Ramadhani. 6. Atayekatiza kufunga Ramadhani, pasi na udhuru wa kisheria, hapati thawabu za kufunga miezi kumi. 7. Mwenye kujiwekea ada ya kufunga Ramadhani kamili, na kufuatiliza kwa kufunga siku sita katika Shawwal, ndiye anayeingia katika thawabu za aliyefunga milele na Dahari katika maisha yake. 8. Ataye fungua katika Mwezi wa Rmadhani, kwa udhuru wa sharia, na akaja kulipa kisheria, ni sawa na aliyefunga kikamilifu Mwezi mzima wa Ramadhani. 9. Wazee wasiojiweza kufunga kwa uzee, au maradhi ya kudumu, na hivyo wakatoa au kutolewa fidia, ni sawa na waliyefunga mwezi mzima wa Ramadhani. 10. Vivyo hivyo, Wazee hao na wagonjwa kama hao, wanaweza vile vile kutolewa Fidia ile ile, kwa ajili ya funga ya Sita, na hivyo kuingia katika wenye kupata thawabu za kufunga mwaka mzima. 11. Kila jema moja, liliotendwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, pekee, basi malipo yake ni malipo ya kufanya mema kumi kama hayo: Na Mwenyezi Mungu huzikuza thawabu hizo, kwa Ampendaye, hadi kufika mia saba: سبحان الله ! ما أكرمك! وما أعظمك! : “Umetakasika, kikomo cha kutakasika, Mola wangu! Ukarimu ulioje na Utukufu ulioje!” 12. Neema na Fadhila za Mwenyezi Mungu hazihesabiki wala hazikadiriki, si kwa makisio wala mahesabu! 13. Fursa za malipo mema ziko nyingi sana; tunazikosa ama kwa ujinga, uzembe, au mapuuza tu. 14. Ramadhani na Sitta ni Msimu Mkubwa wa Kulima kwa wingi, na Kupanda mbegu nyingi kwa mavuno mengi ya baadae. 15. Mwenye kukosa fadhila za Ramadhani na Sitta, amenyimwa kheri nyingi sana. Mwenyezi Mungu Atuwafikishe kukamilisha kuifunga Swaumu ya Mwezi wa Ramadhani, kama Apendavyo, na Atukirimu – kwa Fadhila Zake na ukarimu Wake- kama Anavyostahiki kumkirimu mja Wake, dhaifu, mwingi wa makosa, aliye jawa na Khofu bila ya kukata tamaa ya kupata Rehema Zake. Na Atuwafikishe, vile vile, kufuatilisha kwa Swamu ya Sita, kama Alivyo tuwafikisha kuufunga Mwezi Wake wa Rmadhani. Ewe Mola wetu! Tuitikie kilio chetu! Tukubalie Toba yetu! Tusamehe dhambi zetu; kwani hapana wa kusamehe ila WEWE, Mwingi wa kusamehe, Msamehevu! وبالله التوفيق الحقير عبد القادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم.

No comments