Jua ya kwamba mambo yanayomtoa Muislamu katika Uislamu ni mambo kumi:
Moja: Ni kumshirikisha Allaah Aliyetukuka katika ibada, Anasema Allaah:
“Hakika
Allaah Haghufuri kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa
Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amepotoka
upotofu wa mbali.” (An-Nisaa: 116)
Na Anasema Allaah:
“Hakika
mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na
makazi yake yatakuwa ni Motoni. Na madhalimu hawatopata mwenye kunusuru
yeyote.” (Al-Maaidah: 72)
na miongoni mwa hizo shirki ni kuchinja kwa asiyekuwa Allaah kama anayechinja kwa ajili ya majini au makaburi.
Pili:
Mwenye kufanya baina yake na Allaah viunganishi akawa anaviomba
viunganishi hivyo na kuvitaka uombezi na kuvitegemea, basi hakika mtu
huyo amekufuru kwa makubaliano ya wanavyuoni.
Tatu: Asiyewakufurisha washirikina au akawa ana shaka katika ukafiri wao au akaupitisha (akausahihisha ) ukafiri wao amekufuru.
Nne:
Mwenye kuamini kwamba muongozo wa asiyekuwa Mtume Muhammad (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndio muongozo ulio kamili kuliko
muongozo wa Mtume au ya kwamba hukmu ya mwengine ni bora kuliko hukmu
yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kama yule
anayefadhilisha hukmu za Matwaghuut kuliko hukmu yake Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi mtu huyo ni kafiri.
Tano: Mwenye kuchukia chochote katika aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata akatekeleza amekufuru.
Sita:
Mwenye kufanyia mzaha (shere) kwa chochote katika dini ya Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au akafanya utani katika thawabu
au katika adhabu za Allaah amekufuru. Na dalili ni neno Lake Allaah:
“Sema: Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayaat Zake na Rasuli Wake?” Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” (At-Tawbah: 65-66)
Saba:
Uchawi; na miongoni mwa huo uchawi ni uchawi wa kutenganisha na
kupendanisha basi yeyote mwenye kufanya huo uchawi au akauridhia
amekufuru. Anasema Allaah:
“(hao Malaika wawili) hawamfundishi yeyote mpaka wamueleze: “Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru (kufanya sihiri).” (Al-Baqarah: 102)
Nane: Kusaidiana na kuwa pamoja na washirikina dhidi ya Waislamu, na dalili ni:
“Na yeyote atakayewafanya awliyaa wao; basi hakika yeye ni miongoni mwao. Hakika Allaah Haongoi watu madhalimu.” (Al-Maaidah: 51)
Tisa:
Mwenye kuamini ya kwamba baadhi ya watu wanaweza kutoka katika shari’ah
ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama
vile alivyoweza kutoka Al-Khidhr katika shari’ah ya Muwsaa basi mtu hiyo
ni kafiri.
Kumi: Kuikataa na kuipa mgongo dini ya Allaah Mtukufu na akawa hajifunzi chochote katika dini. Na dalili ni neno Lake Allaah:
“Na nani dhalimu zaidi kuliko yule anayekumbushwa Aayaat za Rabb (Mola) wake, kisha akakengeuka nazo (kuzipuuza)? Hakika Sisi Tutawalipiza wahalifu.” (As-Sajdah: 22)
Na
wala hakuna tofauti katika mambo haya yanayomtoa Muislamu katika Uislamu
kwa yule anayefanya utani au anayefanya kwa kweli au anayeogopa ila
anayetenzwa nguvu (kama kushikiwa silaha na akalizimishwa kufanya mambo
hayo). Na yote hayo tuliyoyataja ni katika mambo makubwa yanayohatarisha
na yanayotokea sana, kwa hivyo yapaswa kwa Muislamu kujihadhari nayo na
ayaogope kwa nafsi yake.
Twajilinda
kwa Allaah kwa yanayopelekea hasira Zake na adhabu Zake kali na rahma
na amani zimfikie kiumbe bora Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) na jamaa zake na Maswahaba wake wote.
No comments