Aliolewa
na Abu Haalah bin Zurarah At-Tamiymiy akamzalia Haalah na Hind
alipofariki Abu Haalah aliolewa na ‘Atiyq bin ‘Aaidhw bin ‘Abdillaah
Al-Makhzuumiy akakaa naye muda kisha wakaachana.
Wakajitokeza
watukufu wengi wa ki-Quraysh lakini aliamua kusimamia malezi ya wanae
na biashara zake Kwani alikuwa tajiri mwenye mali anaajiri wanaume
katika biashara zake na kuwalipa, ilipomfikia habari ya Mtume (Swalla
Allahu ‘alayhi wa sallam) kabla ya utume kwa aliyosifika nayo katika
ukweli, amana na tabia nzuri alimuajiri na kumtuma Shaam na kijana wake
aitwae Maysarah.
Akakubali
Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) akasafiri na Allaah
Akamuwafikisha katika biashara hii akarudi na faida kubwa akajua Bi
Khadiyjah kwamba huyu mwanaume sio kama wengine akaanza kujiuliza je,
kijana huyu atakubali kumuoa mama aliyefikia miaka arobaini? Jamii
itamfikiriaje naye amewakataa wengi?
Alipokuwa
katika lindi la mawazo akaingia rafiki yake Nafiysah bint Manbah na
akaweza kumdodosa mpaka akamueleza linalomsumbua, naye akamtuliza na
kumweleza kuwa yeye ni mwenye cheo, mali, uzuri wanaume wote
wanampigania hivyo asijali naye atamsaidia.
Akatoka kwake na kuelekea kwa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) akaanza mas-ala kwa akili na kumuuliza:
Kitu gani kinakuzuia kuoa ewe Muhammad?
Akajibu sina mkononi cha kuolea… akatabasamu huku akisema:
Je, ukitoshelezeka na kuitwa katika mali, uzuri, utukufu, usawa (kafaa-ah) utakubali? Akajibu kwa kuuliza ni nani? Akajibu kwa haraka ni Bi Khadiyjah bint Khuwaylid.
Akasema ikiwa atawafiki, basi nami nimekubali.
Akarudi
haraka kumpa bishara rafiki yake. Na Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa
sallam) akawaeleza ‘Ami zake kuhusu kumuoa Bi Khadiyjah, Akaenda Abu
Twaalib na Hamzah kwa ‘Ami yake Khadiyjah ‘Amru bin Asad wakamposea na
kutoa mahari.
Akahudhuria
katika sherehe Haliymah Sa’adiyah (mnyonyeshaji wa Mtume Swalla Allahu
‘alayhi wa sallam) wakamzawadia mbuzi arobaini wakati wa kurejea.
Wakaishi
maisha mazuri ya furaha na heshima na wakaajaliwa kupata watoto sita
(Al-Qaasim, ‘Abdullaah, Zaynab, Ruqayyah, Ummu Kulthuum, na Faatwimah)
na neema ikawa inazidi akawa Bi Khadiyjah mke mwema mtiifu mwenye
mapenzi hakumdharau mumewe kwa kuwa na mali tofauti na leo baadhi ya
wanawake wanapokuwa na cheo au mali hawatimizi wajibu wao na wanakuwa na
kiburi.
Alipofikia
Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) miaka arobaini alipenda
kujitenga na watu na kufanya ibada mwezi mzima katika pango akichukua
chakula na wakati mwengine akiletewa na Bi Khadiyjah ambaye hakudhikika
na kupenda kwake kukaa pangoni, alikaa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa
sallam) katika ibada hii kiasi Alichojaaliwa na Allaah kisha akamshukia
Malaika Jibriyl (‘Alayhis Salaam) na kumpa bishara ya Utume katika pango
la Hiraa katika mwezi wa Ramadhaan, akatetemeka na kuogopa kwa kumuona
Malaika huku akimbana na kumtaka asome akasema mimi sijui kusoma
akasema:
“Soma kwa jina la Mola wako…” kisha akasoma Surah ya mwanzo kushuka ambayo ni Iqraa alipoachiwa alifanya haraka kurudi nyumbani huku akisema “nifunikeni, nifunikeni”.
Bi
Khadiyjah alipojua kisa chote alimwambia usiogope Allaah Hawezi
kukutupa Kwani wewe unaunga undugu, unakaribisha wageni na kuwasaidia
wenye matatizo. Ukatulia moyo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam)
akarudi katika hali ya kawaida, hakuishia hapa mke huyu mwenye akili na
hikma bali alimuendea mtoto wa ‘Ami yake Waraqah bin Nawfal na
kumsimulia yaliyompata Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
“Hakika
aliyemuona ni Naamuus (Jibriyl) aliyekuwa anamshukia Nabii Muusa na
‘Iysa naye ni Nabii wa Ummah huu mwambie awe thabiti…”
Akawa
Bi Khadiyjah ni wa mwanzo katika waliomuamini akawa pembeni yake
anamtetea na kumpa moyo anamsaidia ikawa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa
sallam) hapatwi na huzuni au matatizo ila akirudi nyumbani anapata
faraja na huku Aayah za Qur-aan zikiendelea kushuka.
1. Ewe uliyejigubika!
2. Simama uonye!
3. Na Mola wako Mlezi mtukuze!
4. Na nguo zako, zisafishe.
5. Na yaliyo machafu yahame!
6. Wala usitoe kwa kutaraji kuzidishiwa.
7. Na kwa ajili ya Mola wako Mlezi, subiri!
Al-Muddaththir: 1-7
Kuanzia
wakati huo yakabadilika maisha ya Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa
sallam) akaanza maisha mapya yaliyojaa baraka na yenye mashaka vilevile,
akampa habari mke wake mwenye imani kwamba wakati wa kulala na raha
umekwisha.
Akaanza
Bi Khadiyjah kulingania Uislam pamoja na mumewe bega kwa bega.
Akawafisha Allaah wanawe wa kiume Al-Qaasim na ‘Abdullaah udogoni naye
akiwa mwenye subira na kutaraji thawabu kwa Allaah na akamuona shahiydah
wa kwanza katika Uislam Summayyah (Radhiya Allaahu ‘anha) akiwa katika
taabu ya mauti mpaka alipochomwa mkuki na kufa.
Akamuaga
mwanae Ruqayyah (Radhiya Allaahu ‘anha) mke wa ‘Uthmaan (Radhiya
Allaahu ‘anhu) alipoelekea Uhabeshi (Ethiopia) kukimbia maudhi ya
Maquraysh.
Akashuhudia
matatizo mengi na yanayompata Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam)
katika kulingania haki na kushikamana nayo huku akimjibu ‘Ami yake kwa
maneno haya ambayo ameyasimulia Ibn Hishaam katika Siyrah yake,
“WaLlaahi
ewe ‘Ami yangu lau wangeweka jua katika mkono wangu wa kulia na mwezi
kushoto ili niache hili jambo siwezi kuacha mpaka adhihirishe Allaah au
niangamie…” Siyratun-Nabawiyah Ibn Hishaam.
ingawa
wanachuoni wa Hadiyth wamesema maneno hayo kutoka kwa Ya’aquub bin
‘Utbah bin Mughiyrah hayana usahihi ingawa Ibn Hishaam kayaweka kwenye
Siyrah yake.
Na
hivyo ndivyo alivyokuwa Bi Khadiyjah katika kumthibitisha Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Maquraysh walipowawekea vikwazo vya
kisiasa, kiuchumi, kijamii hakusita kusimama na Waislamu katika Shi’ibiy
Abiy Twaalib miaka mitatu huku akiacha nyumba yake, alijitolea mali
yake yote huku akiwa na miaka sitini na tano.
Baada
ya kuisha vikwazo kwa miezi sita alifariki Abu Twaalib kisha akafuatia
Mujaahidah Muhtasibah As-Sayidat Quraysh Atw-Twaahirah (Khadiyjah bint
Khuwaylid (Radhiya Allaahu ‘anha)) kabla ya hijra kwa miaka mitatu.
Ikafuatia
matatizo baada ya kifo cha Bi Khadiyjah kwa Mtume (Swalla Allahu
‘alayhi wa sallam) Kwani alikuwa waziri wa kweli katika Uislam.
Na
hivyo ikaondoka nafsi iliyotulia kwenda kwa Mola ilipofikia ajali yake
baada ya kuacha mfano mwema katika njia ya Da’awah, mke mwema aliyetoa
katika njia ya kumridhisha Allaah akapewa bishara njema ya nyumba
peponi.
Kwa hilo alikuwa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) akisema:
“Bora ya wanawake Maryam bint ‘Imraan, bora ya wanawake Khadiyjah bint Khuwaylid”.
Ee Mola Mridhie Khadiyjah bint Khuwaylid mke mkweli, Muuminah, aliyeipigania Dini kwa kila alichomiliki duniani.
No comments